Manara afunguka ya moyoni

Monday , 17th Jul , 2017

Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara amefunguka kwa mara ya kwanza na kusema anaishukuru kamati kwa kumuondolea adhabu hiyo huku akidai aliyeondolewa adhabu siyo yeye, bali ni Simba na mchezo wenyewe wa soka.

Mkuu wa Kitengo cha Habari wa klabu ya Simba Haji Manara.

Manara amepata msamaha huo baada ya Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kukaa chini kupitia maamuzi mbalimbali ya viongozi wa soka nchini ambao waliwasilisha barua za maombi kutaka kupitiwa tena kwa hukumu zao zilizotolewa hapo awali.

"Leo ni siku kubwa kwa mchezo wa mpira wa miguu nchini hususan washabiki na mchezo huo murua, baada ya kamati ya nidhamu kuitengua adhabu yangu ya kufungiwa mwaka mmoja, kujihusisha na maswala ya kandanda ndani na nje ya nchi.  Adhabu hii ilikuwa inaiumiza sana klabu yangu na kuiondolea haki yake muhimu ya kuwapa habari kwa wakati watanzania juu ya kinachoendelea kwenye klabu", ameandika Manara kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Pamoja na hayo Manara ameendelea kwa kusema "Nitakuwa mjinga nisipowashukuru wanasimba wenzangu ambao siku zote wamekuwa upande wangu, hawa ninawaahid kuwatumikia kwa moyo na dhamira ile ile ya Haji ya kuhakikisha haki na wajibu wetu kama klabu unatekelezwa. Nawaahidi kuendelea kufanya kazi zangu kwa weledi, nidhamu na kwa kuzingatia miiko ya mchezo huu unaobeba dhamana za maisha ya watu walio wengi, sambamba na kuendelea kuitetea na kuilinda klabu yangu kwa nguvu zote", amesisitiza Manara.

Kwa upande mwingine, kikosi cha Simba  kimeondoka nchini asubuhi ya leo kuelekea Afrika ya Kusini kuweka kambi maalum kwa ajili ya kujiandaa michuano ya Ligi kuu inayotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao kwa msimu wa mwaka 2017/2018.