Ijumaa , 27th Aug , 2021

klabu ya Manchester City ya England imejitoa kwenye kinyanganyiro cha kumuwania mchezaji bora wa Dunia mara 5 Cristiano Ronaldo mwenye umri wa miaka 36. Na kwa sasa Klabu ya Manchester United ndiyo inayoripotiwa kuwa kwenye mazungumzo na wakala wa mchezaji huyo Jorge Mendes.

Cristiano Ronaldo

Mabingwa wa England Manchester City ndio waliokuwa wanapewa kipaumbele kumsajili Ronaldo na iliripotiwa kuwa  walikuwa tayari kumpa mkataba wa miaka miwili (2) na mshahara wa pauni 230,000 kwa wiki, lakini kwa mujibu wa taarifa kutoka England Manchester City ndio wamejitoa licha ya kambi ya Ronaldo kuwapa kipaumbele kwenye usajili wa mchezaji huyo.

Kambi ya Ronaldo chini ya wakala wake Jorge Mendes wanaripotiwa kuwa kwenye mazungumzo na Manchester United, taarifa za usajili wa Ronaldo kujiunga na mashetani hao wekundu zitakuwa ni taarifa njema na za furaha kwa mashabiki wa timu hiyo kwani Ronaldo amekuwa mchezaji wao kipenzi baada ya kuitumikia timu hiyo kwa mafanikio kati ya mwaka 2003 hadi 2009 ambapo alitwaa jumla ya mataji tisa (9) katika viunga vya Old Traford ukiwemo ubingwa wa Ligi ya mabingwa Ulaya na ubingwa wa Ligi Kuu England mara tatu (3).