Ijumaa , 30th Sep , 2022

Msemaji wa Simba kupitia akaunti yake ya Instagram amesema moja ya tatizo ambalo wanapaswa kulitatua ni mashabiki wa timu hiyo kutoenda uwanjani kwenye mechi zao za nyumbani

Ally amesema idadi ya mashabiki wanaoingia uwanjani kwenye mechi zao za nyumbani ni ndogo.

"Wengi tunaenda uwanjani kutokana na ukubwa wa mechi au ukubwa wa mashindano ndo maana ni rahisi kujaza uwanja kwenye derby au mechi za kimataifa," amesema Ally na kuongeza;

"Ukienda Old Trafford mechi ya Manchester na Arsenal inajaza uwanja na mechi Manchester na Watford inajaza uwanja hapa mashabiki hawafuati mpinzani wanaifuata timu yao na hiki ndo kilio changu,"

Ally ametolea mfano mechi ya dhidi ya Geita Gold timu hiyo ilipata mapato ya Sh14 milioni tu.

"Ni pesa ndogo mnoo kwenye mpira wa miguu. Kama tunaingiza Sh14 milioni, kwa mechi 14 za nyumbani tutavuna Sh210 milioni  ambayo haitoshi hata mishahara ya mwezi mmoja. Ni rahisi kumsikia mtu anasema kama hamna pesa ya usajili semeni tuchange,"

Ally amesema kuchangishana sio njia ya kudumu ya kuendesha klabu, njia ya sahihi klabu kupata fedha ni mapato ya mlangoni na yanapatikana kwa sisi mashabiki kuja kwa wingi mechi za nyumbani.

Simba itacheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji Jumapili saa 1:00 usiku