Ijumaa , 17th Jul , 2020

Manchester United ndiyo klabu pekee ambayo haijapoteza mchezo kwenye ligi kuu ya soka nchini Uingereza tangu kurejea kwa ligi hiyo, Mwezi Juni mwaka huu, ikishinda mechi tano na sare mbili kwa wastani wa pointi 2.43 kwa kila mchezo.

Marcus Rashford na Antony Martial kwa pamoja wakishangilia baada ya kufunga bao.

 

Ushindi wa 2-0 dhidi ya Crystal Palace kwenye uwanja wa Selhurst Park, ulifunika machungu ya mechi ya Jumatatu, pale Southampton waliposawazisha dakika za lala salama na kuirudisha nyuma United kwenye mbio za kumaliza nne bora.

Huu ni mchezo 19 kwenye michuano yote kwa mashetani wekundu hao bila kupoteza ambapo wamekuwa na kiwango kizuri katika eneo la mwisho la umaliziaji kwa wachezaji wake ambao wanachagizwa na kiungo fundi Bruno Fernandes.

Penginge unaweza jiuliza,kipi kimeleta mabadiliko haya kwa kasi kubwa bila ya kutegemewa?

A-Kiwango cha kiungo matata Bruno Fernandez.

Kiwango kizuri cha Fernandes wenyewe wanamuita Fernandiesta , kinazoeleka ndani ya kikosi cha United na unaweza kusema Mreno huyo aliitawala game dhidi ya Crystal Palace na amekuwa na furaha kucheza eneo hilo la kati kama mtu muhimu wa kupeleka mashambulizi kwenye upande wa timu pinzani.

Tukiingalia zaidi mechi ya Alhamisi mabao yote mawili pasi zilianzia kwa kwake alipotengeneza mpira uliofika miguuni kwa Marcus Rashford ndani ya penati box kinda huyo akawagalagaza walindi wa Palace na kuipa uongozi United wa bao la kwanza dakika ya 45.

Goli la pili likaanzia tena kwa Bruno akipenyeza tena pasi ya mahaba kwenye miguu ya Rashford ambaye akaususa mpira ili uende kwa Antony Martial aliyetumbukiza kambani na kuiandikishia United bao la pili dakika ya 78.

Fernandes sasa ana ana pasi nne za mabao tangu kurejea kwa ligi, ikiwa ni idadi ya juu kuliko mchezaji mwingine yeyote kwenye kipindi hiki, lakini pia akifunga mabao 5 na kumweka nafasi ya nne katika orodha hiyo ya ufungaji.

Haina ubishi kwa sasa Fernandes ndiye mchezaji muhimu kwenye ligi kuu ya soka nchini Uingereza akitengeneza mabao mengi kwa timu yake .

B-Miujiza ya mshambuliaji wa kifaransa Antony Martial.

Kama Fernandez ni mfalme wa United kwa sasa, pia Martial  anaweza kuwa nyota wa 2020, akifunga jumla ya mabao 12 kwenye mashindano yote kumi kati ya hayo ni kwenye premier league akilingana na Mohamed Salah ambaye naye anaidadi hiyo ya makumi mawili nakukumbusha hii ni baada ya kurejea kwa ligi.

Kulikuwa na changamoto kwa Mfaransa huyo kwenye eneo la kucheza hasa akizoea kutokea kushoto, kwenye nafasi ambayo pia Rashford hupendelea kucheza.

Lakini kwa sasa hilo limekwisha na wachezaji hao wawili wanaelewana wakiwa dimbani wanakuwa wanabadilisha kulingana na aina ya mashambulizi na jinsi ya kujipanga.

 
Kwa taarifa yako tu,Rashford na Martial kwa ujumla wameingia kwenye orodha ya tano bora ya vinara ya upachikaji mabao katika EPL,kila mmoja akiwa na mabao 17,maana yake wote wameshafunga mabao 34 msimu huu wa ligi ya England.

Kwa sasa huwezi kuwaacha kuwazungumzia wachezaji watano muhimu kwa United ambao wanachangia timu hiyo kupata ushindi.

Na ndio maana bao la pili dhidi ya Cystal Palace Rashford akalitengeneza kwa Martial.

Mashabiki wameanza kuburudika kama ile enzi ya Sir Ferguson akiwatumia mapacha Andy Cole na Dwight Yorke katika kutengeneza mabao.

Mbali na Fernandes, Rashford na Martial, lakini kuna Paul Pogba injini ya timu eneo la kupelekea timu juu, na dogo wa miaka 18 Mason Greenwood anayetokea wingi ya kulia wametoa mchango mkubwa kwenye kikosi cha Mashetani wekundu hao.

Kwa takwimu halisi tangu kurejea kwa ligi,Manchester United ndiyo timu bora ya pili nyuma ya Manchester City kwa kukusanya alama katika EPL,ikiwa na alama 17 katika michezo saba waliyoteremka dimbani.

Man City wana alama 18,wakifuatiwa na Chelsea nafasi ya tatu huku bingwa Liverpool akishika nafasi ya tisa akiwa na alama 11.

Kwa kiwango hiki cha sasa cha United unaweza kuipeleka kwenye nafasi ya nne kwa mechi hizi mbili zilizobaki Julai 22 dhidi ya West Ham na Julai 26 dhidi ya Leicester anayekomaa kwenye nafasi hiyo hiyo ya nne.