Jumamosi , 3rd Mar , 2018

Klabu ya soka ya Yanga imetoa utaratibu kwa mshabiki wake wanaotaka kusafiri na timu hiyo kwenda jijini Gaborone nchini Botswana kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya timu ya Township Rollers.

Mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya timu hizo utachezwa uwanja wa taifa jijini Dar es salaam siku ya Jumanne Machi 6 huku mechi ya marudiano ikitarajiwa kupigwa wiki moja baadae.

Mashabiki hao watalazimika kulipa kiasi cha Dola 489 zaidi ya shilingi milioni moja ili kusafiri kwa ndege, ikiwa ni gharama za kwenda na kurudi japo haijawekwa wazi kama gharama hizo zinahusika na malazi, chakula pamoja na tiketi za mchezo.

Yanga imetinga hatua hiyo ya kwanza kwenye michuano hiyo baada ya kuiondoa klabu ya St. Louis ya Shelisheli kwenye mchezo wa hatua ya awali ambapo Yanga ilishinda kwa jumla ya mabao 2-1 katika mechi mbili za nyumbani na ugenini.