Ijumaa , 25th Jul , 2014

Kocha mkuu wa klabu ya Yanga Marcio Maximo asema anachokiangalia ni mchezaji kujitoa kwa ajili ya timu na kuonesha uwezo wa kuisaidia timu pamoja na kuwa na nidhamu ya hali ya juu nje na ndani ya uwanja na hatoangalia rekodi wala ukubwa wa jina

Wachezaji Hamis Kiiza na Emmanuel Okwi wakishangilia, ambapo mmoja wao atatupiwa vilago msimu huu

Kocha mkuu wa klabu ya soka ya Yanga Mbrazil Marcio Maximo amesema haumii kichwa juu ya maamuzi ya kupunguza mchezaji mmoja wa kimataifa miongoni mwa washambuliaji wawili raia wa Uganda Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza ambao wako katika majukumu ya timu yao ya taifa "The Cranes"

Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza wameingia katika kapu la uhenda mmoja wao akatupiwa vilago baada ya Yanga hivi karibuni kufanya usajili wa mshambuliaji Mbrazil Genilson Santos Santana 'Jaja' na hivyo kutishia mustakabali wa mmoja kati ya washambuliaji hao wawili raia wa Uganda huku kukiwa na taarifa ambazo si rasmi zikidai uhenda mshambuliaji mtukutu na mwenye uwezo mkubwa dimbani Emmanuel Okwi ndiye akawa mbuzi wa kafara hasa kutokana na hali ya mvutano baina yake na viongozi wa kalabu hiyo na hata tabia ya kuikacha timu hiyo huku ikiwa na michezo muhimu ya ligi kuu na yeye kutimkia nchini kwao

Maximo amesema watu wengi wamekuwa wakijiuliza ni jinsi gani atafanya maamuzi hayo mazito lakini kwake si tatizo kwani ana taarifa za wanandinga hao na hivyo yeye atafuata falsafa yake ya nidhamu mbele na timu kwanza mchezaji baadaye na kamwe hata angalia ukubwa wa jina la mchezaji husika.