Jumatano , 9th Aug , 2017

Mgombea urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ali Mayay amesema kuwa katika uongozi wake atahakikisha dira ya mpira wa miguu inarejea katika mstari na kuiwezesha nchi kupata maendeleo makubwa kupitia sekta hiyo.

Mayay amesema hayo leo alipokuwa ananadi sera zake katika siku ya kwanza ya uzinduzi wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa TFF utakaofanyika Agosti 12, mkoani Dodoma na kusema kuwa kwa sasa hakuna dira ya mpira wa miguu na ndiyo chanzo cha kuwa na maendeleo duni ya mpira kulinganisha na nchi zingine ambayo kwa sasa zinafaidi matunda baada ya kuanzisha na kutekeleza dira hiyo.

“Kwa sasa wachezaji wengi wa Zambia wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi, timu yao Taifa inafanya vizuri, Tanzania ina wachezaji wengi wenye vipaji, lakini hakuna dira na kusababisha wao pia kukosa dira katika fani yao,” alisema Mayay.

Mayay ameongeza kuwa akiwa kama mchezaji wa zamani, ameona changamoto mbalimbali za mpira wa miguu na kuamua kugombea nafasi iliyo ili kuzitatua na lengo lingine ni kujenga taasisi imara kwa kutumia rasilimali zilizopo kwani tatizo si vipaji, bali ni aina gani ya uongozi unaosimamia mpira wa miguu.

Hata hivyo Mayay amekuwa akiungwa mkono na wachezaji wenzake wa zamani huku wakidai kuwa, Mayay ni dira ya soka Tanzania, kwa kuwa amecheza soka kuanzia shuleni hata katika vilabu mpaka timu ya Taifa hivyo atajua nini cha kufanya ili kuleta maendeleo ya soka.