Jumamosi , 1st Aug , 2020

Klabu ya soka ya Mbao Fc imeporomoka kutoka ligi kuu hadi daraja la kwanza kufuatia kuondoshwa na Ihefu ya Mbeya kwa matokeo ya jumla ya sare ya 4-4.

Mshambuliaji wa Mbao Fc, Waziri Junior akishangilia moja ya bao lake alilofunga katika mchezo dhidi ya Ihefu ingawa haikutosha kuwanusuru kushuka daraja

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza, Ihefu ilipata ushindi wa bao 2-0 katika uwanja wake wa Nyumbani lakini katika mchezo wa marudiano uliopigwa CCM Kirumba jijini Mwanza,wenyeji waliibuka na ushindi wa bao 4-2 lakini kwa mujibu wa kanuni,Ihefu inasonga mbele kutokana na kupata mabao ya ugenini.

Mbao Fc ilipanda ligi kuu msimu wa mwaka 2016 baada ya kashfa ya upangaji matokeo ambayo ilipelekea vilabu vya JKT Kanembwa,Jkt Oljoro, Polisi Tabora kushushwa daraja na wao kuibuka vinara katika kundi lao.

Wakati huo huo klabu ya Mbeya City imesalia ligi kuu baada ya kuinyuka Geita Gold bao 1-0 na hivyo kushinda kwa jumla ya bao 2-1 katika michezo miwili.

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza, mbeya City ilitoka sare ikiwa ugenini ya bao 1-1 kabla ya jioni ya leo kupata ushindi muhimu wa bao 1-0 ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.