Jumanne , 23rd Jul , 2019

Moja ya vihoja vinavyozua gumzo katika tasnia ya soka hivi sasa ni suala la mchezaji aliyepewa zawadi ya kuku kwa kuibuka mchezaji bora wa mchezo.

Mchezaji wa Nyasa Big Bullets, Hassan Kajoke akikabidhiwa kuku

Hiyo imetokea nchini Malawi katika mchezo wa Ligi Kuu nchini humo wikiendi iliyopita kati ya klabu ya Nyasa Big Bullets na Karonge United, ambao ulimalizika kwa Nyasa Big Bullets kuibuka na ushindi wa mabao 5-0, huku mshambuliaji Hassan Kajoke akiibuka kama mchezaji bora kufuatia mabao mawili ambayo alifunga.

Taarifa za awali zilidai kuwa zawadi hiyo ya kuku ilitolewa na mdhamini wa ligi hiyo, lakini baada ya kuzua gumzo mitandaoni, Shirikisho la Soka nchini Malawi likajitokeza na kueleza kuwa kuku alitolewa na shabiki ambaye alivutiwa na kiwango cha mchezaji huyo.

Klabu ya Nyasa Big Bullets iliweka picha ya mchezaji huyo katika ukurasa wake wa Facebook, ikionesha wakati akipokea zawadi hiyo na kumtaja shabiki aliyetoa kuku huyu kwa jina la Mapale palibenso kuwa alivutiwa na kiwango cha mchezaji huyo mpaka akaamua kumzawadia kuku, jambo ambalo limezidi kuzua gumzo katika mitandao ya kijamii lakini baadaye iliondolewa.