Jumatano , 3rd Apr , 2019

Mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na JKT Tanzania uliokuwa upigwe katika dimba la Jamhuri mjini Morogoro, umeahirishwa kutokana na mvua.

Basi la Simba

Mvua kubwa iliyonyesha mchana mjini Morogoro, imesababisha Uwanja wa Jamhuri kujaa maji kiasi cha mpira kushindwa kudunda. Baada ya kusubiri kwa nusu saa, wasimamizi wa mechi wakaamua kuahirisha na kuahidi kuupangia ratiba nyingine.

Charles Mwakambaya ambaye ni Katibu wa chama cha soka mkoani Morogoro na msimamizi wa TFF kituo cha Morogoro, akizungumza baada ya mchezo kuahirishwa amesema kuwa hawatoweza kuipangia ratiba Simba kucheza kesho kwa sababu ya mchezo wa Klabu Bingwa Afrika, Jumamosi dhidi ya TP Mazembe.

"Hatuwezi kusema kuwa mchezo uchezwe kesho kwa sababu Simba ina ratiba ya mchezo wa TP Mazembe Jumamosi hii, kwahiyo wakicheza kesho tutakuwa tumwanyima masaa 48 ya kujiandaa dhidi ya mchezo mwingine", amesema Mwakambaya.

Kuhusu mashabiki ambao walishalipia tiketi zao, Mwakambaya amesema kuwa hela hazitorudishwa lakini utafanyika utaratibu mzuri na mambo yatakuwa sawa kwa mashabiki hao.

Simba sasa itarejea Jijini Dar es salaam kujiandaa na mchezo huo wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ambao inaelezwa kuwa wameshatua nchini.