Alhamisi , 12th Sep , 2019

Nahodha wa Barcelona, Lionel Messi ameweka wazi kuwa alikuwa ana matarajio makubwa juu ya usajili wa Neymar Jr katika klabu yake msimu huu.

Lionel Messi na Neymar Jr

Muunganiko wa raia hao wa Amerika Kusini ulidumu kwa miaka minne wakicheza kwa pamoja katika safu ya ushambuliaji Camp Nou, ingawa Mbrazil huyo alibadili njia na kujiunga na Ligue 1 katika klabu ya PSG mnamo mwaka 2017 kwa lengo la kutafuta ufalme wake mpya na kuepuka kuwa katika kivuli cha Messi.

Wakati wa muda wao pamoja katika viunga vya Catalonia, Messi alifunga jumla ya mabao 196, ambayo ni 91 zaidi ya Neymar.

Akizungumzia kuhusu tetesi za Neymar kutaka kurejea Barcelona ambazo ziligonga mwamba dakika za mwisho, Messi amesema, "nitapenda sana kuona Neymar akirejea tena. Ninaelewa kuwa kuna watu wanapinga urejeo wake na inajulikana kilichotokea hadi Neymar akaamua kuondoka".

"Mimi nafikiri Neymar ni mmoja wa wachezaji bora sana duniani na kuwepo kwake ndani ya kikosi chetu kutaongeza ari ya kupigania malengo yetu. Lakini mwisho wa siku haikuwezekana kurejea, kwa sasa tunatakiwa kufikiria zaidi juu ya kikosi tulichonacho pamoja na malengo tuliyojiwekea", ameongeza Messi.

Tetesi za Neymar kutaka kurejea Barcelona zilipamba moto katikati mwa dirisha kubwa la usajili, ikielezwa kuwa Barcelona walikuwa tayari kuwatoa wachezaji wao watatau muhimu, Osmane Dembele, Ivan Rakitic na Todibo. Lakini dili hilo lilikufa baada ya PSG kukataa kumuachia mshambuliaji huyo japokuwa mwenyewe alikuwa tayari kuondoka.