Ijumaa , 23rd Apr , 2021

Mshambuliaji na nahodha wa FC Barcelona Lionel Messi ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao 25 kwenye ligi kuu nchini Hispania kwa micimu 12 mfululizo, mshambuliaji huyo amefikia rekodi hiyo baada ya kufunga mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Getafe.

Messi

Mabao mawili aliyofunga Messi yamemfanya afikishe mabao 25 msimu huu kwenye La Liga na ndio kinara wa ufungaji akiwa anaongoza kwa tofauti ya mabao 4 dhidi ya Karim Benzema wa Real Madrid mwenye mabao 21.

Baada ya kufikia idadi hiyo ya mabao kwenye ligi kuu Hispania sasa Messi anakuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya ligi hiyo kufunga mabao 25 au zaidi ya idadi hiyo kwa msimu wa 12 mfululizo, pia akiwa ndio mchezaji pekee kufanya hivyo kwenye ligi kubwa tano barani ulaya.

Lakini pia raia huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 33, amefunga mabao 23 kwenye michezo 23 ndani ya mwaka 2021. Na mpaka sasa amefikisha jumla ya mabao 33 msimu huu kwenye mashindano yote katika michezo 41.

Na ushindi huo wa Barcelona umewafanya wafikishe alama 68 wakisalia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa La Liga, Atletico Madrid ndio vinara wakiwa na alama 70 wakati Real Madrid wapo nafasi ya pili wakiwa na alama 70 lakini vilabu hivyo vya jiji la Madrid vimecheza mchezo mmoja zaidi ya Barcelona ambao wamecheza michezo 31.