Jumanne , 3rd Dec , 2019

Usiku wa kuamia leo Desemba 3, 2019, jijini Paris Ufaransa zilitolewa tuzo za Ballon d'Or, ambapo katika tuzo ya mchezaji bora, mshindi aliibuka nyota wa Barcelona na Argentina Lionel Messi.

Messi akiwa na tuzo zake 6 za Ballon d'Or

Nyota huyo alitangazwa mshindi na mshereheshaji wa tuzo hizo ambaye alikuwa mshambuliaji wa zamani wa Chelsea na Ivory Coast Didier Drogba, hivyo kumfanya Messi afikishe tuzo 6 za Ballon d'Or na kuwa mchezaji mwenye tuzo hizo nyingi zaidi.

Katika kuwania tuzo hiyo Messi alikuwa anashindana na mpinzani wake wa muda mrefu Cristiano Ronaldo ambaye ni mshindi mara tano wa tuzo hiyo, pamoja na mlinzi wa Liverpool na Uholanzi Virgil van Dijk.

Miaka ambayo Messi ameshinda tuzo hiyo ni kuanzia mwaka 2009, ambapo alishinda mara 4 mfululizo hadi mwaka 2012, aliposimamishwa na Ronaldo ambaye alibeba 2013 na 2014 kabla ya Messi tena kushinda 2015.

Mwaka 2016 na 2017 Ronaldo akashinda tena na mwaka 2018 kwa mara ya kwanza tuzo hiyo ikaenda nje ya wachezaji hao wawili katika kipindi cha miaka 10, ambapo kiungo wa Real Madrid na Croatia Luka Modric alitwaa.

Mwaka 2019 Messi ameshinda tena tuzo hiyo, ambapo imeelezwa kuwa amesaidiwa na takwimu zake binafsi kutonana na timu yake ya Barcelona kushinda taji la La Liga pekee huku yeye binafsi akiibuka mfungaji bora barani Ulaya.

Katika tuzo hizo, mchezaji bora kijana chini ya miaka 21 ni Matthijs de Ligt wa Juventus ambaye alikuwa na mwaka mzuri akiwa na Ajax na Uholanzi. Golikipa bora alikuwa ni Alisson Becker wa Liverpool na Brazil.