Alhamisi , 23rd Sep , 2021

Bondia kutoka Ukraine Oleksander Usyk, ametupilia mbali kauli za watu wanaombeza kuelekea pambano la jumamosi dhidi ya Anthony Joshua, inayohusisha mikanda ya uzani mzito wa IBF,WBA na WBO pambano litakalofanyika kwenye dimba la Tottenham.

Oleksander Usyk

Bondia huyo ambaye amewahi kushinda medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Olimpiki, amesema kuwa wanaobeza uwezo wake na umbo lake kuwa ni dogo hawapo sahihi kwakuwa mchezo wa ngumi unahusisha maandalizi pamoja na iman ya bondia apandapo ulingoni, akitoa mfano wa David Haye aliyemtwanga Nikolai Valuev akiwa na umbo ndogo mara tatu la mpinzani wake.

Usyk anakutana na kauli hizo kutokana na kukosa uzoefu wa mapambano ya uzani mzito baada kupanda kutoka uzani wa kati akiwa na mapambano machache tangu apande uzani huo.

Usyk anawania kuwa bondia wa tatu katika historia ya masumbwi, baada ya Evander Holyfield na David Haye, kushinda mataji ya ulimwengu kwa uzani wa kati na pamoja na uzani mzito.

Kwa upande wa Anthony Joshua amesema anahitaji kucheza mchezo huo kwa ubora mkubwa licha ya kuwa na umri wa miaka 31, huku akiamini kuwa anaweza kufanya vizuri kwa kuwa anahamasishwa na kinachofanywa na mchezaji wa Manchester United, Cristiano Ronaldo mwenye umri wa miaka 37.