Jumamosi , 14th Jul , 2018

Nahodha wa timu ya Kikapu ya St. Joseph Etiene Elijjah Ismael, amesema mwakani wanampango wa kuongeza timu kwenye michuano ya Sprite Bball Kings kutokana na kuwepo kwa wachezaji wengi wa mchezo huo chuoni hapo ambao hawawezi kucheza katika timu moja.

Timu ya Kikapu ya St. Joseph

Akiongea na www.eatv.tv Etiene amesema wanashukuru baada ya kushiriki msimu uliopita wakapenda mashindano wakaamua kuanzisha timu ya pili ambayo ni DMI, lakini wameona mwakani pia watengeneze timu ya tatu kutokana na baadhi ya wachezaji kuendelea kukosa nafasi katika timu hizo mbili.

''Mashindano ni mazuri nawaomba tu wadau wazidi kujitokeza kushuhudia mechi za robo fainali maana ndio wanatupa nguvu ya kuzidi kufanya vizuri na kuongeza timu. Kama sisi hapa chuoni tuna timu mbili ambazo zimeingia hatua hiyo sisi na timu ya DMI na tunataka kuongeza ya tatu mwakani'', - amesema.

St. Joseph na DMI zote zinatokea chuo cha St. Joseph na zimetinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo na inatarajiwa kufanyika Julai 21 kwenye uwanja wa ndani wa taifa ambapo St. Joseph watacheza na mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars huku DMI wakicheza na Team Kiza.

Mshindi wa michuano hiyo inayoandaliwa na East Africa Television LTD na kudhaminiwa na kinywaji cha Sprite, atajinyakulia zawadi ya shilingi milioni 10 huku mshindi wa pili akipata milioni 3 na MVP milioni 2. Mechi za robo fainali zitaanza Saa 6:00 mchana hadi saa 2:00 usiku.