Jumanne , 13th Feb , 2018

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ameyataka mashirikisho ya Sanaa na Filamu kusimamia ubora wa kazi za sanaa ili kukidhi mahitaji ya walaji.

Akiongea na viongozi wa Mashirikisho hayo leo ofisini kwake Mwakyembe amewataka kusimamia ubora kwani ndio kitu pekee kitawafanya mashabiki kuzipenda filamu za nyumbani.

"Ongezeni juhudi katika kusimamia uboreshaji wa kazi za sanaa na filamu ili ziweze kuthaminiwa na kukidhi matakwa ya walaji kwa kuwafanya kupenda vya kwetu", amesema.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bibi. Joyce Fisoo ameyataka Mashirikisho ya sanaa na filamu kufuata na kusimamia sheria, kanuni na taratibu za kutafsiri kazi za filamu za nje kwa kuwa na kibali cha mmiliki wa filamu.

Naye Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa Bibi. Leah Kihimbi, ameyaasa mashirikisho ya Sanaa na Filamu nchini kusimamia vyema vyama vilivyopo chini ya mashirikisho hayo ili kuhakikisha shughuli zote za sanaa zinapita kwenye mashirikisho husika.