Mwakyembe kumkutanisha Infantino na Magufuli

Jumanne , 13th Feb , 2018

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ameahidi kufanya jitihada za kumkutanisha Rais wa FIFA Gianni Infantino na Rais Magufuli kwaajili ya kujadili namna ya kuendeleza soka nchini.

Hayo ameyasema leo wakati akiongea na wahariri wa michezo nchini ambapo ameeleza kuwa Rais Magufuli ni mpenda michezo hivyo atafanya jitihada zake zote kuhakikisha anakutana na Rais Infantino atakapokuja nchini kwenye mkutano maalumu wa FIFA.

''Kwakuwa Rais Magufuli ni mpenda michezo, lazima atapenda kuonana na Rais wa FIFA Gianni Infantino, na mimi kama waziri mwenye dhamana ya michezo nitahakikisha hilo linawezekana'', amesema.

Aidha Dkt. Mwakyembe amewaeleza wahariri kuwa maandalizi ya mkutano huo yamekamilika na wameandaa mazingira mazuri ya wageni kufikia kuanzia mapokezi na huduma zingine. Mkutano huo wa Mwaka utashirikisha mataifa 19 na utafanyika Februari 22 katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam. 

Mwenyekiti wa mkutano huo ni Rais wa FIFA Gianni Infantino huku wageni wengine kama Katibu Mkuu wa FIFA, Fatma Samba Diouf Samoura na Sekretarieti ya FIFA pamoja na rais wa CAF, Ahmad Ahmad wanatarajiwa kufika.