Jumanne , 14th Aug , 2018

Mwamuzi bora wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu uliopita Eli Sasii, ameteuliwa kuamua mchezo wa Ngao ya hisani kati ya Simba na Mtibwa Sugar utakaopigwa Agosti 18, 2018 kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mwamuzi Eli Sassi (kulia).

Mwenyekiti wa Kamati ya waamuzi ndani ya shirikisho la soka Tanzania ( TFF ), Salum Omande Chama, amesema Sasii atasaidiwa na mwamuzi bora msaidizi wa msimu uliopita Hellen Mduma pamoja na Ferdinand Chacha.

Chama ameiambia East Africa Radio kupitia kipindi cha Kipenga kuwa, maandalizi kwa upande wa waamuzi yamekamilika na wote watatua Mwanza mapema kwaajili ya taratibu zingine kuelekea mchezo huo.

Mchezo huo ambao huwakutanisha bingwa wa ligi kuu soka Tanzania ambaye kwa msimu uliopita ni Simba SC na bingwa wa kombe la shirikisho ambaye ni Mtibwa Sugar, ni ishara ya kufunguliwa kwa ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2018/19 inayoanza Agosti 22.