
Nahodha msaidizi wa klabu ya Simba, Mohamed Hussein ''Tshabalala'' katika Uwanja wa Bunju (Mazoezini)
Tshabalala ambaye ndiye alikuwa nahodha wa Simba katika mchezo wa jana waliofungwa na Prisons kwa bao 1-0, alikubali pia walipoteza mchezo licha ya kutengeneza nafasi nyingi lakini hawakuzitumia.
''Unajua wewe unapoacha kucheza, wenzako wanacheza na wanapata matokeo, kitu hicho kinawaongezea kujiamini na muendelezo mzuri kimbinu na kimfumo. Kwakweli mechi zetu kusimamishwa imetuathiri' alisema Tshabalala.
Klabu ya Simba ilipaswa kucheza na Yanga Oktoba 18 lakini bodi ya ligi ilisogeza mbele dabi hiyo hadi Novemba 7 mwaka huu kutokana na hofu ya vikwazo vya usafiri kwakuwa baadhi ya wachezaji walisafiri kuzitumikia timu zao za taifa ikiwa ni changamoto ya Covid-19.
Simba ilipoteza mchezo wa kwanza wa VPL msimu huu na wamebaki katika nafasi ya tatu wakiwa na alama 13 huku Yanga ambao walishinda dhidi ya Polisi Tanzania, wameketi katika nafasi ya pili nao Azam wakiendelea kukamata usukani wakiwa na alama 21.