Jumapili , 19th Jun , 2016

Kwa wale wanaofuatailia na kuitazama kwa ukaribu michuano ya mpira wa kikapu nchini Marekani NBA hasa katika michezo ya fainali zake ni wazi atakili ni mchuano mkubwa baina ya miamba LeBron James na Stephen Curry ambao wamekuwa wakizisaidia timu zao

Wachezaji Le Bron James na Stephen Curry kuamua bingwa wa NBA

Mfalme LeBron James mara nyingi amekuwa akiwika na kufanya vema na kuonyesha maajabu ama kufanya miujiza ya mchezo huo na mara hii sasa anasubiriwa kuona akifanya ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya ligi kuu ya mpira wa kikapu nchini Marekani maarufu kama NBA.

Katika historia ya michuano ya NBA haijawahi kutokea timu ikatwaa ubingwa wa michuano hiyo baada ya awali kuanza kwa kupoteza michezo mitatu ya awali ya fainali katika nne za kwanza kati ya saba za michuano hiyo, lakini nyota James ana nafasi ya kuweka rekodi hiyo ya kihistoria msimu huu baada ya kuiwezesha Cleverland Cavaliers kuzinduka kutoka nyuma katika kipigo cha michezo mitatu kwa moja [3-1] nakushinda michezo miwili mfululizo dhidi ya wapinzani wao Golden State Warriors na hatimaye kulazimisha kuchezwa kwa mchezo wa saba wa fainali hizo.

Mchezo wa saba [game 7] ya fainali hizo za NBA utapigwa leo usiku wa kuamkia kesho kwenye uwanja wa Warriors Oracle Arena Mjini Oakland.

Rekodi ya ubora wa James katika mchezo uliopita aliweza kufunga kwa mara ya pili mfululizo pointi 41 huku akitoa mipira ya msaada [assist] 11, akiwahi mipira ribaundi 8, akiiba mipira mara 4 na kupiga mipira ya kuzuia mara tatu[block 3], wakati mpinzani wake Stephen Curry wa Golden State Warriors yeye akitupia pointi 30, akiwahi mipira yaani ribaundi tatu, akitoa msaada [assist] 1 na kuiba mpira mara 1.

Hivyo usiku wa leo kuamkia kesho alfajiri utakuwa ni usiku wa rekodi kwa miamba hiyo na hasa baada ya mchezo wa juzi kuishia kwa Cavaliers kuibuka na alama ya vikapu 115- 101.