Jumatatu , 4th Mei , 2026

 Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), limemteua Mwamuzi kutoka DR Congo, Jean-Jacques Ndala, kusimamia mchezo wa awamu ya kwanza wa fainali ya CAF Champions League kati ya Mamelodi Sundowns na FAR Rabat.

Jean-Jacques Ndala - Mwamuzi kutoka DR Congo

Klabu ya Sundowns kutoka Afrika Kusini itakuwa mwenyeji wa mchezo huo utakaopigwa Mei 17, 2026 katika Uwanja wa Tshwane-Loftus Versfeld, kabla ya marudiano kufanyika wiki moja baadaye nchini Morocco.

Ndala atasaidiwa na waamuzi wenzake kutoka DR Congo, Guylain Bongele Ngila na Mwanya Gradel Mbilizi, huku Messie Jessie Oved akiteuliwa kuwa mwamuzi wa akiba (fourth official).

Uteuzi wa Ndala unaonesha imani kubwa ya CAF kwa uwezo wake wa kusimamia mechi za presha kubwa. Katika miaka ya karibuni, amehudumu katika michezo mingi muhimu ya kimataifa ikiwemo ligi ya mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, akipongezwa kwa utulivu, uthabiti na umakini wake uwanjani.

Kwa Ndala, hii ni hatua nyingine muhimu katika taaluma yake, kwani kuchezesha fainali ya mashindano makubwa kama haya ni heshima kubwa kwa mwamuzi yeyote barani Afrika. Utendaji mzuri unaweza kuimarisha zaidi nafasi yake miongoni mwa waamuzi bora kabisa wa bara hili.