Patrick Aussems afafanua kuhusu kuondoka kwake

Jumanne , 19th Nov , 2019

Kocha mkuu wa Simba Patrick Aussems, ameweka wazi kuwa alilazimika kuondoka nchini kwa siku mbili kutokana na mambo yake binafsi.

Kocha wa Simba Patrick Aussems (kulia) akikumbatiana na mchezaji Miraji Athumani

Aussems amefafanua hilo muda mfupi baada ya EATV & EA Radio Digital kuwasiliana na Mtendaji mkuu wa Simba Senzo Mazingiza na kuthibitisha kuondoka kwa Aussems.

Kupitia mtandao wa Twitter Aussems amesema, 'Ni kweli nililazimika kuondoka kwa siku mbili kwa masuala yangu binafsi, narejea kesho Jumatano tayari kwa maandalizi ya mchezo wetu wa ligi kuu wikiendi hii dhidi ya Ruvu Shooting'.

Aussems pia amesema kuwa ana imani katika mchezo huo wataendelea kuvuna pointi tatu muhimu. Simba kwasasa inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 22 kwenye mechi 9.