
Uganda dhidi ya Tanzania
Kilimanjaro Stars inaingia katika hatua ya nusu fainali baada ya kufanikiwa kuvuka katika kundi B pamoja na timu ya Kenya ambayo iliongoza kundi huku Uganda ikivuka kutoka katika kundi A pamoja na Eritrea.
Rekodi ya michezo baina ya timu hizo inaonesha kuwa zitakutana katika mchezo wa 22 kwenye michuano hiyo, ambapo Uganda Cranes ikiwa imeshinda mechi 13, ikifungwa katika mechi tatu na kutoka sare kwenye michezo mitano.
Kocha wa Uganda, Jonathan McKinstry amesema, "Tanzania ni nchi ya mpira, wana ushindani mkubwa kwahiyo kama tunahitaji kushinda leo tunatakiwa kuonesha kiwango chetu bora. Tanzania ina wachezaji bora ambao wanaweza kutuadhibu pia".
Naye kocha wa Kilimanjaro Stars, Juma Mgunda amesema, "tunawaheshimu Uganda na tunafahamu kuwa ni wenyeji wa michuano kwahiyo wanapewa nafasi kubwa lakini tutapambana mpaka mwisho, hatutawaogopa. Najua watakuwa na sapoti ya mashabiki wao lakini tutafanya kadri ya uwezo wetu ili tufike fainali".
Kilimanjaro Stars ni mabingwa mara tano wa michuano hiyo huku Uganda Cranes wakiwa ndio mabingwa mara nyingi, wakifanikiwa kushinda ubingwa mara 14.
Mchezo wa mapema leo wa nusu fainali utashuhudia mabingwa watetezi Kenya wakivaana na Eritrea.