Jumatatu , 16th Jul , 2018

Pambano la uzito wa juu la kuwania mikanda ya ubingwa wa dunia kati ya mabondia Anthony Joshua anayelinda mikanda yake ya IBF, WBA (Super), WBO na IBO dhidi ya Alexander Povetkin anayeshikilia mkanda wa WBA (Regular) limetangazwa kufanyika Septemba 22, 2018.

Bondia Anthony Joshua

Pambano hilo ambalo litapigwa kwenye uwanja wa Wembley jijini London nchini Uingereza, linatarajiwa kuwa na ushindani kutokana na mabondia hao kubobea kwenye upande wa 'KO'. Joshua ana rekodi ya kushinda kwa KO mapambano 20 kati ya 21 huku Povetkin ameshinda mara 24 kwa KO kati ya 34.

Joshua mwenye umri wa miaka 28 ana rekodi ya kutopoteza pambano hata moja tangu aanze kupigana akiwa ameshinda mapambano yote 21 aliyopanda ulingoni huku mpinzani wake Povetkin mwenye miaka 34 akiwa na rekodi ya kupoteza pambano 1 kati ya 35 aliyopigana.

Joshua atakuwa anarejea kwenye uwanja wa Wembley kwa mara ya kwanza tangu alipopigana pambano la mwisho  dhidi ya Wladimir Klitschko April 2017 ambapo mashabiki 90,000 walihudhuria pambano hilo lililomalizika kwa Joshua kushinda kwa 'TKO'.

Bondia Alexander Povetkin

Kabla ya pambano la Septemba 22, Joshua amepigana mara mbili dhidi ya Carlos Takam na Joseph Parker mapema mwaka huu na alishinda yote kwa KO. Kwa upande wake Povetkin pambano la mwisho alishinda kwa KO dhidi ya David Price wa Uingereza. 

Mshindi wa pambano hilo atabeba mikanda mitano ya uzito wa juu yaani minne ya IBF, WBA (Super), WBO  na IBO aliyonayo Joshua na ule mmoja wa WBA (Regular) alionao Povetkin.