Jumatatu , 17th Jan , 2022

Kuelekea mchezo wa leo kati ya Mbeya City dhidi ya Simba SC katika dimba la Sokoine, rekodi zimeendelea kuitesa wagonga nyundo wa jiji la mbeya, ambapo katika mechi tano zilizopita, wamefungwa mitanange yote kwa jumla ya mabao 13 huku wao wakifunga magoli mawili tu.

Simba wanaingia katika michezo wa leo wakiwa na ushindi wa 4-1, 0-1, 0-2, 4-0, 1-2 vile vile msimu huu wakiwa na kikosi kamili kilichosheni nyota kama Clatous Chama aliyejiunga na Wekundu wa Msimbazi akitokea RS Berkane.

Kutokana na rekodi hizo benchi la ufundi la Mbeya City limetamba kuwa licha ya ubora walionao wapinzani wao lakini watahakikisha wanapata ushindi.

Mchezo huo wa ligi unatarajiwa kupigwa leo Januari 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Meneja wa Mbeya City, Mwegane Yeya, amesema: “Tunaendelea na maandalizi kuelekea kwenye mchezo wetu wa ligi dhidi ya Simba.

“Tunajua Simba wana timu nzuri, wachezaji wazuri kutokana na ubora waliouonyesha kwenye michuano ya Mapinduzi lakini hata sisi pia tuna kikosi bora, hivyo tutahakikisha tunapata ushindi kwenye mchezo huo".

“Utakuwa mchezo mgumu lakini sisi haitutishi, tutahakikisha tunautumia vizuri uwanja wetu wa nyumbani kwa kupata pointi tatu kama ikishindikana basi tupate pointi moja kuliko kupoteza.” alisema meneja wa Mbeya City