Alhamisi , 19th Sep , 2019

Nyota wa klabu ya Juventus, Cristiano Ronaldo amezungumzia historia ya ndani ya maisha yake kipindi alipokuwa anaanza kucheza soka nchini Ureno. 

Cristiano Ronaldo

Akizungumza na ITV Football, Ronaldo amesema kuwa alipokuwa na miaka 10 au 11 mjini Lisbon nchini Ureno, hakuwa na pesa za kumuwezesha kuishi na alikuwa akiishi sehemu moja na wachezaji wenzake katika kambi.

Katika kipindi hicho alipokuwa kambini Jijini Lisbon, wazazi wake walikuwa wakiishi mjini Madeira na alikuwa akiwatembelea kila baada ya miezi mitatu kutokana na hali ya maisha ya wazazi wake kutokuwa nzuri.

"Ilikuwa ni kipindi kigumu sana kutokuwa karibu na wazazi. Tukiwa kambini, majira ya usiku wa saa 4:30 au saa 5 tulikukuwa tukihisi njaa, kwahiyo tulikuwa tukielekea katika mgahawa mmoja karibu na uwanja wetu ambapo tulikuwa tukienda kugonga mlango na kuuliza kama chakula kimebakia", amesimulia Ronaldo.

"Edna na wasichana wengine wawili walikuwa wakarimu kupitiliza, sikuweza kuwaona tena wale wasichana. Ninajaribu kuongea na watu mbalimbali nchini Ureno ili kufahamu walipo na nina imani kupitia majohiano haya, itasaidia kuwapata", ameongeza.

Ronaldo amesisitiza kuwa anataka kukutana na wasichana hao ili aweze kuwarudishia kitu kutokana na mafanikio yake hivi sasa. Anataka kuwaalika nyumbani kwake wapate chakula pamoja. 

Aidha katika majohiano hayo ambayo mwenyewe amesema ndiyo ya kwanza kwake kumtoa chozi, Ronaldo amezungumzia jinsi anavyomkumbuka baba yake ambaye amefariki dunia, akisema kuwa anatamani baba yake angekuwepo kipindi hiki ashuhudie mafanikio aliyo nayo pamoja na tuzo mbalimbali anazozipata.