Jumapili , 6th Dec , 2020

Winga wa kimataifa wa Tanzania Simon Msuva, jana Disemba 6, 2020, ametambulishwa kwenye timu yake mpya ya Wydad Casablanca ya nchini Morocco na kukabidhiwa jezi namba 11.

Winga wa kimataifa wa Tanzania Simon Msuva

Akiongea baada ya uitambulisho, Msuva ambaye ametoa klabu ya Difaa Hassani El Jadidi ya Morocco, amesema sababu ya kuchukua jezi hiyo ni kutokana na namba 27 kuwa na mtu.

Aidha ameongeza kuwa ana furaha na namba 11 kwasababu ni sehemu ya heshima kwa mchezaji wa zamani wa Simba SC Musa Mgosi ambaye aliwahi kumtabiria kuwa atafika mbali sana.

“Alisikia kuwa kuna kijana anaitwa Simon anajua sana mpira ndio akataka anione, alivyoniona kuna maneno akaniambia wewe kijana unajua sana mpira lazima utafika mbali na alinipa zawadi ya jezi yake namba 11 ya Simba nikawa naenda nayo kwenye Ndondo”, amesema  Simon Msuva.

Msuva aliondoka Tanzania msimu mwaka 2018 na kujiunga na Difaa Hassani El Jadidi ambako amecheza misimu miwili na sasa amejiunga na miamba hiyo ya soka barani Afrika kwa mkataba wa miaka minne.