Jumanne , 12th Nov , 2019

Nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta, amesema kitendo cha kukutana njiani na mchezaji Simon Msuva wakiwa wote wanakuja nyumbani kulitumikia taifa, kimemfurahisha sana.

Mbwana Samatta akiwa amembeba Simon Msuva kwenye moja ya mechi za Taifa Stars.

Akiongea baada ya kutua kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa na Simon Msuva, amesema amefurahi kukutana Ulaya na Msuva na anatamani waongezeke wengine.

'Namuomba Mungu baada ya miaka mitatu tuwe tunakutana Ulaya wachezaji hata 7 au 8 tunakuja kuliwakilisha taifa', amesema Samatta.

Kwa upande wa mchezo unaokuja wa kuwania kufuzu AFCON dhidi ya Equatorial Guinea, Samatta amesema yupo tayari kwa mchezo huo na watahakikisha wanatumia vizuri uwanja wa nyumbani.

'Tutahakikisha tunafanya vizuri, sijui sana kuhusu taifa hilo na wachezaji wake lakini sisi tupo tayari na hatutaki kukosea kama mwaka ule tuliposhindwa kuwafunga nyumbani Lesotho kitu ambacho baadaye tulikijutia sana', amesema.

Taifa Stars itacheza na Equatorial Guinea Novemba 15,2019 kuwania kufuzu AFCON 2021. Mchezo utapigwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es salaam.