Samatta atoa ujumbe kwa watanzania baada ya AFCON

Jumatano , 3rd Jul , 2019

Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta amesema kuwa wao kama wachezaji walifurahia kupata nafasi ya kushiriki AFCON 2019 na walikuwa na lengo la kufanya vizuri.

Mbwana Samatta kwenye mchezo dhidi ya Algeria

Samatta kupitia ujumbe wake maalum kwenye mitandao ya kijamii alioutoa leo Julai 3, 2019, amesema wametimiza ndoto ya watanzania kufuzu lakini hali halisi imeamua matokeo waliyopata.

''Ilikuwa ni ndoto ya kila mtanzania kuona tunashiriki michuano ya AFCON na sote tulifurahia kupata nafasi hii. Tunafahamu watanzania walitamani timu ifanye vizuri na kufika mbali, hata sisi wachezaji hilo lilikuwa lengo letu namba moja lakini hali halisi imefuta ndoto zetu'', amesema.

Ameongeza kuwa ''Tunawashukuru mashabiki wote mliotuunga mkono katika kipindi chote kuanzia maandalizi hadi leo, nawaomba mfahamu tu kuwa hili lilikuwa darasa tosha kwetu sote. Ulikuwa ni wakati wa kila mmoja wetu kwa nafasi yake kujifunza kitu''.

Samatta ambaye aliiongoza Stars katika mechi tatu za kundi C ambazo zote walipoteza dhidi ya Senegal, Kenya na Algeria amewataka watanzania waendelee kushikamana.