Jumapili , 26th Mei , 2019

Mshambuliaji wa klabu ya Genk na nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta amewaahidi Watanzania kuwa atajitahidi kwa uwezo wake kuongoza vyema Taifa Stars katika michuano ya mataifa ya Afrika, AFCON mwezi ujao nchini Misri.

Mbwana Samatta

Amesema hayo baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere alfajiri ya leo na kupokewa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akitokea nchini Ubelgiji katika klabu yake ya Genk.

Samatta ambaye ameonesha kiwango cha juu msimu huu katika michuano ya Europa League na Ligi Kuu nchini Ubelgiji, amesema kuwa anafahamu jukumu ambalo Watanzania wamewakabidhi kuelekea michuano ya AFCON  na yeye kama nahodha na wachezaji wenzake wameahidi kuwa watapambana hadi mwisho.

"Baada ya muda mrefu sana tumepata nafasi hii ya kwenda kushiriki, ukweli ni kwamba ni uzoefu mkubwa sana tunakwenda kuupata kutokana na uchanga wa timu yetu ya taifa kwa sababu hatujakuwepo kwenye mashindano kwa muda mrefu", amesema Samatta.

"Mpira siku zote una matokeo ya kushangaza, inawezekana tukawa wachanga kwa sababu ya muda mrefu kutoshiriki lakini tukafanya vizuri. Mimi kama kampteni naichukua timu yangu, tunaenda kushiriki na kupambana kuhakikisha tunapata kitu", ameongeza.

Pia Samatta amezungumzia juu ya ndoto yake ya kucheza soka nchini Uingereza, ambapo amesema, "huwezi jua kinachokuja mbele lakini mimi siku zote toka nikiwa mtoto tulikuwa tunaenda kwenye mabanda ya kuonesha mpira na nilikuwa mmoja wapo ambaye nilikuwa napenda kuangalia EPL, ni kitu ambacho kinanivutia sana. Napenda kucheza ligi ya Uingereza lakini huwezi jua itakuwaje".