Jumatatu , 3rd Feb , 2020

Mshambuliaji wa klabu ya Aston villa na timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Mbwana Samatta ameeleza masikitiko yake kufuatia maoni yasiyoridhisha ya Watanzania katika mitandaao ya kijamii.

Mbwana Samatta

Samatta amesema hayo kufuatia Watanzania kutoa maoni yasiyoridhisha yakiwemo matusi katika kurasa za klabu ya Aston Villa na kurasa za wachezaji wa timu hiyo, wakidai kuwa mchezaji wao hapewi nafasi nyingi uwanjani.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Samatta ameandika, "mashabiki wa soka Tanzania nafahamu kuwa mnanipenda kijana wenu na mnapenda nifanye vizuri katika timu yangu mpya, lakini nawaomba muache kutoa maneno ya kashfa au yenye mlengo mbaya katika kurasa za timu au wachezaji, binafsi sifurahishwi".

Aston Villa ilicheza mechi ya ligi wikiendi iliyopita dhidi ya AFC Bournemouth ambayo pia ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa Samatta katika Ligi Kuu nchini Uingereza na kufanikiwa kufunga bao, licha ya timu yake kupoteza kwa mabao 2-1.

Tangu Samatta atue Aston Villa, mashabiki na Watanzania wengi wamekuwa wakiifuatilia kwa ukaribu klabu hiyo mtandaoni. Ambapo tangu tetesi za usajili wake zilipoanza, takribani wafuasi 170,000 wameongezeka katika mtandao wa Instagram.