Jumanne , 19th Feb , 2019

Mambo yanazidi kumuendea kombo kocha wa Chelsea, Muitaliano, Maurizio Sarri baada ya kupigwa mechi ya pili kati ya tatu za karibuni hapo jana dhidi ya Man United.

Kocha Maurizio Sarri na Mmiliki wa klabu, Roman Abramovich

Katika mchezo huo wa kombe lenye heshima zaidi nchini Uingereza, FA Cup, imeshuhudiwa Manchester United ikiiadhibu Chelsea kwa mabao 2-0 katika dimba la Stamford Bridge, mabao yaliyofungw ana Ander Hererra na Paul Pogba.

Ni wazi kuwa matokeo hayao mabaya yanazidi kumchanganya mmiliki wa klabu hiyo, bilionea wa Urusi, Roman Abramovich ambaye amekuwa si mvumilivu kwa makocha wake hasa katika kipindi kigumu kama hiki ambacho ameanza kupitia kocha wake.

Katika miaka 15 iliyopita, Abramovich amebadilisha makocha takribani 9 klabuni hapo huku wengi wao wakiondoka kwa sababu ya mwenendo mbaya wa matokeo, ambapo maamuzi mengine yaliwaacha mashabiki midomo wazi, mfano alipomfukuza kocha Roberto Di Matteo muda mfupi baada ya kuisaidia Chelsea kushinda taji la kwanza la Klabu Bingwa Ulaya kwa kuifunga Baryern Munich mwezi Mei mwaka 2012.

Mwenyewe Maurizio Sarri ameeleza baada ya mchezo huo kuwa alichokuwa akihofia alipokuwa nchini Italia ni matokeo na sio kelele na kejeli za wadau na mashabiki wa soka, hali ambayo hadi hivi sasa inampa mwanga wa kujiamini na kazi yake katika klabu ya Chelsea.

"Nilikuwa na wasiwasi nilipokuwa katika ligi daraja la pili nchini Italia, na sio sasa. Nilihofia zaidi kuhusu matokeo na sio mashabiki na nilielewa juu ya hali iliyopo", amesema Sarri.

"Tunafahamu kuwa tumetupwa nje ya mashindano, ninaelewa juu ya hali ya mashabiki, nina wasiwasi juu ya matokeo yetu", ameongeza.

Tetesi za hivi karibuni zimezidi kumpa shinikizo kocha huyo aliye na msimu mmoja tu klabuni hapo, kwani amekuwa akihusishwa kocha wa zamani wa Real Madrid, Zinedine Zidane kuchukua nafasi yake huku mwenyewe Zidane akiweka wazi masharti yake ili aweze kujiunga na klabu hiyo.