Jumamosi , 2nd Jul , 2016

Kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya Tanzania waliochini ya umri wa miaka 17 Serengeti Boys hii leo imefanikiwa kuiondosha Shelisheli katika mchezo wa marudiano kuwania tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana AFCON U17

Serengeti Boys wakiwa katika moja ya mazoezi yao jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda Shelisheli.

Timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imeshinda mabao 6-0 dhidi ya Shelisheli katika mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza kuwania tiketi ya kufuzu kwa fainali za vijana U17 Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Madagascar mchezo uliofanyika jioni ya leo Uwanja wa Stade Linite mjini Victoria.

Kwa matokeo hayo, Serengeti Boys inasonga mbele na kwenda raundi ya Pili na hatua ya mwisho ya mchujo kwa ushindi wa jumla wa mabao 9-0 baada ya wiki iliyopita kushinda 3-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa katika uwanja wa Taifa,jijini Dar es Salaam.

Serengeti Boys sasa itamenyana na Afrika Kusini, ikumbukwe hiyo ni kama marudio ya mchezo wa mwaka jana katika hatua hiyo hiyo, ambayo vijana wa Tanzania walitolewa.

Mashujaa wa Serengeti Boys katika mtanange huo ambao walipachika mabao hayo ya Serengeti hii leo nipamoja na Shaaban Zubeiry akifunga bao dakika ya saba, Mohammed Abdalah dakika ya 49, Hassan Juma ambaye alipachika mabao mawili dakika ya 47 na 75, Issa Makamba yeye akifunga kwa mkwaju wa penati kunako dakika ya 65 na msumali wa mwisho uligongelewa na Yohana Nkomola kunako dakika ya 90 na kufanya ubao wa matangazo kusomeka Serengeti Boys 6 wenyeji Shelisheli 0.