Alhamisi , 12th Mei , 2016

Timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys imetua salama jijini Goa, India kwa ajili michuano maalumu ya soka ya kimataifa kwa vijana (AIFF Youth Cup 2016 U-16) yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini humo (AIFF).

Mkuu wa msafara wa timu hiyo, Ayoub Nyenzi amesema kwamba wamepokelewa vizuri na wenyeji India na leo asubuhi Mei 12, 2016 wachezaji watapumzika kabla ya baadaye saa 10.00 jioni kuanza kujifua kwa mazoezi mepesi.

Kikosi hicho cha wachezaji 22, kiko chini ya Kocha Bakari Shime na kinaundwa na makipa, Ramadhan Kabwili, Kelvin Kayego na Samwel Brazio wakati mabeki wa pembeni ni Kibwana Shomari, Nicson Kibabage, Israel Mwenda na Ally Msengi.

Mabeki wa kati ni Issa Makamba, Nickson Job na Ally Ng'anzi huku viungo wakiwa ni Maulid Lembe, Asad Juma, Kelvin Naftari, Yasin Mohamed na Syprian Mwetesigwa na washambuliaji ni Aman Maziku, Rashid Chambo, Enrick Nkosi, Yohana Mkomola, Mohamed Abdallah, Shaban Ada na Muhsin Mkame.

Michuano hiyo inatarajiwa kuanza leo Mei 12, 2016 kwa mfumo wa ligi kwa timu tano kucheza mechi nne, Tanzania itafungua dimba dhidi ya Marekani kwenye Uwanja wa Tilak Maidan, Vasco, Goa huku mchezo wa pili ukiwa kati ya wenyeji India dhidi ya Malysia Mei 15, mwaka huu.

Serengeti Boys watashuka dimbani tena Mei 17, kucheza na wenyeji India mchezo wa kwanza, Mei 19 Serengeti Boys watacheza dhidi ya Korea Kusini na mchezo wa mwisho watamaliza dhidi ya Malaysia Mei 21.

Fainali ya michuano hiyo itachezwa Mei 25 ambapo kabla ya mchezo wa fainali, utachezwa mchezo wa mshindi wa tatu katika uwanja huo huo Tilak Maidan, Vasco, Goa nchini India.