Silaha tatu za Man City zarejea

Jumatatu , 12th Feb , 2018

Kuelekea mchezo wa ligi ya Mabingwa Barani Ulaya UEFA nyota watatu wa Manchester City waliokuwa majeruhi wamerejea kwenye mazoezi ya jumatatu jioni tayari kwa maandalizi ya kuivaa FC Basel kesho.

Wachezaji waliorejea leo ni winga Leroy Sane, kiungo David Silva na mlinzi Fabian Delph ambao walikuwa wameumia kwa nyakati tofauti.

Sane aliumia mguu kufuatia kuchezewa rafu mbaya na mchezaji Joe Bennett wa Cardiff City katika mchezo wa Kombe la FA ambapo Man City ilipata ushindi na kusonga mbele. Silva aliumia goti kwenye ushindi wa 3-0 iliopata City dhidi ya West Brom.

Delph aliumia goti kwenye mchezo wa EPL ambapo Man City ilipoteza kwa mara ya kwanza 4-3 dhidi ya Liverpool Januari 14.

Man City itakuwa ugenini kucheza na FC Basel kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya 16 ligi ya mabingwa Ulaya. Matajiri hao wa jiji la Manchester wanaongoza ligi ya EPL wakiwa na alama 72.