Ijumaa , 11th Dec , 2015

Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara inarejea kesho baada ya mapumziko ya takriban mwezi mzima kupisha mechi za timu ya taifa na michuano ya Kombe la CECAFA Challenge.

Nyasi za viwanja sita zitawaka moto kesho, lakini macho na masikio ya wengi vitaelekezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambako vigogo Simba SC watakuwa wanamenyana na vinara wa Ligi Azam FC.

Azam FC wanahitaji ushindi katika mchezo wa kesho kujiimarisha kileleni na kuzidi kuwaacha mabingwa watetezi, Yanga SC wakati Simba SC inahitaji ushindi ili kurudi kwenye mbio za ubingwa.

Mabingwa watetezi, Yanga SC wao kesho watakuwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kumenyana na timu ngumu, MGambo JKT ya Kabuku, Tanga ambapo Kagera Sugar wataikaribisha Ndanda FC Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora.

Stand United wakiongozwa na kinara wa mabao Ligi Kuu, Elias Maguri wataikaribisha Mwadui FC ambapo Mbeya City wataikaribisha Mtibwa Sugar huku Majimaji wakiikaribisha Toto Africans.

Michuano hiyo itaendelea Jumapili kwa kwa kupigwa michezo miwili ambapo JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Karume na Coastal Union watamenyana na mahasimu wao, African Sports.