Jumanne , 13th Feb , 2018

Vinara wa ligi kuu soka Tanzania Bara Simba SC iliyopo kileleni mwa msimamo na mabingwa watetezi Yanga SC iliyopo nafasi ya pili zinatarajiwa kucheza mechi zao za viporo za VPL kabla ya kusafiri kwa mechi za kimataifa.

Yanga ambayo haikucheza mchezo wake wa raundi ya 18 kutokana na wikiendi ililiyopita kucheza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya St. Lousi ya Shelisheli, itaikaribisha Majimaji FC kwenye uwanja wa Uhuru.

Simba wao hawakucheza mchezo wao wa raundi ya 18 kutokana na kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika ambapo walicheza na Gendarmerie ya Djibouti. Alhamisi watakuwa mjini Shinyanga kucheza na Mwadui FC.

Tayari Yanga wameshaweka wazi kuwa watasafiri siku ya Jumapili Februari 18 kuelekea Shelisheli kwaajili ya mchezo wa marudiano utakaopigwa Februari 21. Simba bado hawajatangaza lini wataondoka nchini.

Simba wanaongoza ligi wakiwa na alama 41 huku wapinzani wao wa Alhamisi Mwadui wakiwa katika nafasi ya 12 na alama 18. Yanga ina alama 34 katika nafasi ya tatu huku Majimaji wakiwa nafasi ya 14 na alama 14.