Jumanne , 12th Feb , 2019

Klabu ya soka ya Simba imeshinda mchezo wake wa pili nyumbani baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly na kufanya kundi D litawaliwe na hesabu kali kuelekea robo fainali.

Wachezaji wa Simba wakishangilia bao dhidi ya Al Ahly leo.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es salaam bao pekee la Simba limefungwa na Meddie Kagere dakika ya 65 ya mchezo.

Ushindi huo umeifanya Simba sasa ifikishe pointi 6 katika mechi 4 hivyo kuwa katika nafasi ya 2 ya kundi D ikisubiri matokeo ya mchezo mwingine wa kundi hilo kati ya JS Sauora dhidi ya AS Vital utakaopigwa majira ya saa 4:00 usiku.

Kundi sasa linaongozwa na Al Ahly wenye pointi 7 katika mechi 4 huku Simba wakiwa nafasi ya pili na pointi 6, AS Vital wakiwa nafasi ya tatu na pointi 4 huku JS Sauora wakishika mkia na alama 2.

Simba itasafiri kucheza mechi yake ya 5 dhidi ya JS Sauora huko Algeria wakati ambao Al Ahly itakuwa ugenini kucheza na AS Vital.