Simba yarejea ligi kuu, hii hapa ratiba ya viporo

Jumatatu , 15th Apr , 2019

Baada ya kuondolewa katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, klabu ya Simba imerejea nchini ikiwa na kazi moja ya kupambana katika ligi kuu.

Simba

Simba ambayo imekuwa na viporo takribani 10 hivi sasa , imereja nchini baada ya kutolewa na TP Mazembe katika robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-1 mjini Lubumbashi.

Katika msimamo wa ligi, Simba inakamata nafasi ya tatu ikiwa na jumla ya pointi 57 baada ya kushuka dimbani michezo 22, ikiwa nyuma michezo 9 dhidi ya Yanga inayoongoza ligi kwa sasa baada ya kucheza mechi 31.

Ratiba ya Simba inaanza Jumatano hii, April 17, ambapo itasafiri hadi jijini Tanga kuvaana na Coastal Union kabla ya kusafiri hadi mkoani Kagera kucheza na Kagera Sugar, mchezo utakaopigwa April 20.

April 23, Simba itasafiri hadi jijini Mwanza kucheza na Alliance FC kisha April 26 kucheza na KMC. Tarehe 28 April itasafiri hadi mkoani Mara kucheza na Biashara United kabla ya Mei mosi kucheza na Tanzania Prisons jijini Mbeya. Ratiba hiyo ya viporo itamalizika Mei 5 kwa kucheza na Mbeya City huko huko jijini Mbeya.