Jumanne , 6th Jan , 2015

SIMBA SC imefanikiwa kufuzu hatua ya Robo fainali za Kombe la Mapinduzi kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKU katika mchezo wa kundi C uliofanyika Uwanja wa Amaan Zanzibar.

Matokeo hayo yanaifanya Simba imalize kileleni mwa kundi C kwa Pointi zake Sita baada ya mechi Tatu mbele ya Mtibwa Sugar iliyomaliza kwa Pointi Tano.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika Simba wakiwa tayari wamepata bao hilo lililofungwa na Ramadhani Singano dakika ya 12 kwa shuti kali akiwa ndani ya Boksi baada ya kupewa pasi nzuri na Said Ndemla.

Timu zote zilishambuliana kwa zamu katika kipindi cha kwanza ambapo timu zote zilikuwa zikipata nafasi za kuweza kufunga lakini zilishindwa kutumia vizuri nafasi hizo.

Kipindi cha pili, mchezo ulizidi kunoga, Simba SC inayofundishwa na Mserbia Goran Copunovic ikisaka mabao zaidi na JKU wakitafuta la kusawazisha.

Hata hivyo Simba walifanikiwa kuulinda Ushindi wao na kusonga mbele, ambapo sasa wanasubiri matokeo ya mwisho katika mechi za leo, kujua mpinzani wao katika hatua ya Robo Fainali.

Mechi za leo zitawakutanisha KCCA na KMKM, AZAM Fc na MTENDE, huku YANGA ikikutana na SHABA Uwanja wa Amaan wakati Uwanja wa Mao dze Tung POLISI itamenyana na Taifa Jang'ombe.