Jumatano , 2nd Jan , 2019

Klabu ya soka ya Simba imezua gumzo katika mji wa Méridja, ambapo ndipo makao makuu ya klabu ya soka ya JS Saoura ya nchini Algeria.

Mohamed Hussein akishangilia na mashabiki

Simba imezua gumzo kubwa kuelekea mchezo wao wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya klabu hiyo, utakaopigwa Januari 12 katika uwanja wa taifa Jijini Dar es salaam.

Katika ukurasa wa Facebook wa klabu ya JS Saoura, kumekuwepo na picha pamoja na video kadhaa tangu tarehe ambayo droo ya hatua ya makundi ya michuano hiyo ilipofanyika, Desemba 28.

Siku moja baada ya droo ya hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Afrika, klabu hiyo ilipandisha video fupi ya mashabiki wa Simba wakishangilia katika mchezo wake na Nkana Red Devils katika uwanja wa taifa, iliyoambatana na maneno yanayoonesha kushangazwa na namna Simba ilivyojaza mashabiki katika uwanja huo.

Maneno hayo yaliendelea kusema kwamba, inashangazwa kuona klabu ya soka inavyojaza uwanja wake namna ile kushinda hata timu ya taifa, huku ikitolea mfano katika mchezo wa Tanzania na Algeria uliofanyika katika uwanja wa taifa kwamba haukuwa na mashabiki wengi kiasi hicho.

Simba imepangwa kundi D katika michuano hiyo, ikiwa pamoja na timu za Al Ahly, AS Vita Club na klabu hiyo JS Saoura ya nchini Algeria ambayo ilianzishwa mwaka 2008.