Jumatatu , 22nd Jan , 2018

Kocha wa Singida United Hans Van Pluijm amesema wachezaji wake wamejiandaa vyema kisaikolojia kuhakikisha wanashinda mchezo wao wa leo jioni dhidi ya Majimaji na kuishusha Yanga SC kwenye nafasi ya tatu.

Akiongea leo Mkurugenzi wa Singida United Festo Sanga amesema kocha Hans ameongea na wachezaji na kuwaondoa hofu huku akiwataka kucheza kwa kujiamini na ana imani watafuata maelekezo na wataibuka na ushindi.

''Hans ni mwalimu mkubwa, amesema hataki kuwaona wachezaji wakicheza kwa presha, ameongea nao na amewataka wacheze bila presha na watapata matokeo mazuri ikizingatiwa klabu inataka kuendelea kuwa katika nafasi za juu'', amesema Festo kwa niaba ya kocha Hans.

Aidha Sanga amethibitisha kuwa kikosi cha Singida United kimefika salama mjini Songea na kimefanya mazoezi kwa siku mbili hivyo wachezaji wako vizuri kwaajili ya mchezo huo wa ligi kuu.

Singida United yenye alama 23 baada ya mechi 13 ikishika nafasi ya tano, endapo itashinda mchezo wa leo itafikisha alama 26 na kupanda hadi nafasi ya tatu, ikizishusha klabu za Yanga SC na Mtibwa Sugar zenye alama 25 katika nafasi za tatu na nne.