Alhamisi , 26th Jul , 2018

Shirikisho la mpira wa kikapu Tanzania, TBF limetangaza kikosi cha taifa kitakachoshiriki michuano ya, 3*3 Africa Qualifiers Basketball Championship yatakayofanyika nchini Madagascar.

Mchezaji, Jovin Charles, akiwa peke yake na katika kikosi cha Dream Chaser.

Mchezaji, Jovin Charles wa timu ya Dream Chaser iliyoshiriki michuano ya  Bball Kings inayoandaliwa na EATV kwa udhamini wa kinywaji cha Sprite ametajwa katika kikosi hicho ambacho kitasafiri kesho Ijumaa.

Jovin Charles aliiongoza Dream Chaser hadi katika hatua nzuri kwenye michuano ya mwaka uliopita licha ya kutolewa katika hatua ya mchujo mwaka huu

 Hadi sasa michuano ya Sprite Bball Kings ipo katika hatua ya nusu fainali, michezo yake ikitarajiwa kupigwa Jumapili hii kati ya Flying Dribblers  na Team Kiza katika nusu fainali ya kwanza huku nusu fainali ya pili ikizikutanisha Portland na Mchenga Bball Stars.

Akitaja kikosi hicho cha taifa, Rais wa TBF, Phares Magesa pamoja na mambo mengine amewaomba wadau wa michezo nchini kuusapoti mchezo huo ili uweze kukua na kuitangaza nchi kimataifa.

Nichukue fursa hii kuishukuru serikali kupitia kwa baraza la michezo la taifa kwa kutuwezesha kufanikisha hili lakini pia nitoe wito tu kwa wadau wengine washirikiane nasi TBF ili kupitia kikapu tuweze kuwakuza vijana wetu", amesema Magesa.

Wachezaji walioitwa katika kikosi ni, Abba Patrick Robert, Haji Rashid Mbegu, Charles Albert Mayombo, Rashid Tariq Maarifa, Jovin Charles Ngowe, Mwalimu Heri Kijogoo, Baraka Nsaji, Phinias Stephen Kashabi na Jonas Mushi, wakiongozwa na meneja na mkuu wa msafara Karabani Lawrence Karabani, kocha Robert Manyerere na afisa wa timu Shabani Mohobonya.