Jumapili , 22nd Feb , 2015

Timu ya Taifa ya Tanzania ya mpira wa ufukweni leo imefanikiwa kuiondoa Kenya katika mbio za kusaka nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, kwa mchezo huo baada ya kuifunga kwa mabao 7-6.

Meneja wa Timu ya Tanzania Deo Lucas, amesema kuwa siri ya ushindi huo ni maandalizi mazuri kabla ya kukutana na Kenya, ambao walikutana nao wiki jana katika mji wa Mombasa na Tanzania ikiwa ugenini ikaibuka na ushindi wa jumla ya mabao 5-3.

Deo amesema kuwa wapinzani wao Kenya walikuwa wazuri zaidi tofauti na mchezo wa kwanza walipokutana kitu ambacho kilifanya mchezo kuwa mgumu sana kwao licha ya kupata ushindi mnono.

Kutokana na ushindi huo Tanzania imesonga mbele kwa jumla ya mabao 12 kwa 9 ,Mwezi Machi kikosi hicho kitasafiri hadi nchini Misri kucheza mchezo wa awali kabla ya kurudiana baada ya wiki moja.

Endapo Tanzania itafanikiwa kuwafunga na kuwaondoa Misri basi moja kwa moja itakuwa imetinga katika fainali za Mataifa ya Afrika ambayo kilele chake itakuwa mwezi Aprili mwaka huu katiika visiwa vya Shelisheli.

Mchezaji wa Tanzania Ally Rabbi amefunga mabao manne pekee na kuipa timu yake ushindi huo mnono.