Jumamosi , 4th Aug , 2018

Nusu fainali ya Sprite Bball Kings inaendelea leo Agosti 4, kwenye uwanja wa ndani wa taifa ambapo 'game 2' zitapigwa huku timu za Team Kiza na Portland zikiwa na nafasi moja tu ya kusawazisha au kuaga mashindano baada ya kupoteza 'game 1'.

Wachezaji wa Mchenga Bball Stars (kijani) na Portland (nyeupe kwenye nusu fainali game 1.

Team Kiza wanaingia uwanjani dhidi ya Flying Dribblers wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza 'game 1' kwenye zile 'best of three' kwa pointi 84 kwa 70, hivyo leo watakuwa wanatafuta ushindi pekee ili kufufua nafasi yao ya kucheza fainali.

Kama watafanikiwa kushinda leo basi watafanya nusu fainali iende  hadi 'game 3' ambapo mshindi ndio atakwenda fainali. Endapo Flying Dribblers watashinda leo watakwenda fainali kwa mara ya kwanza baada ya mwaka jana kutolewa katika nusu fainali na Mchenga Bball Stars.

Kwa upande wa Portland nao wapo kwenye mtihani kama wa Team Kiza baada ya kuruhusu kufungwa  pointi 70 kwa 54 na Mchenga Bball Stars kwenye 'game 1' ya 'best of three'. Leo wanahitaji matokeo ya ushindi pekee ili kuitafuta game 3 ambayo itaamua timu gani inakwenda fainali.

Mechi za leo zinaanza saa 10:00 jioni zikiambatana na burudani mbalimbali ikiwemo muziki pamoja na kinywaji baridi cha Sprite ambao ndio wadhamini wa michuano hii. Watakaofuzu fainali watakwenda kupigania milioni 10 kwa bingwa na milioni 3 kwa makamu bingwa pamoja na milioni 2 kwa MVP.