Jumanne , 10th Jul , 2018

Timu ya mpira wa Kikapu ya Temeke Heroes ambayo imetinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Sprite Bball Kings, imesema kwasasa Temeke imeendelea kwenye mchezo wa Kikapu tofauti na zamani ambapo ilitambulika zaidi kwa mchezo wa soka.

Kikosi cha Temeke Heroes

Akiongea baada ya droo ya robo fainali iliyofanyika jana usiku, nahodha wa timu hiyo Rajabu Mikingi alisema wao wapo kwaajili ya kuiwakilisha Temeke kwenye michuano ya Sprite Bball Kings na wanaamini kuwa wataibuka mabingwa na kujinyakulia kitita cha shilingi milioni 10.

''Tumejipanga kuendelea kufanya vizuri na sasa tumewajua wapinzani wetu wa robo fainali ambao ni Portland, tunawaheshimu ni timu bora na wamefanya vizuri kwenye mechi yao ya 16 bora lakini hiyo haitutishi Temeke kwasasa tupo vizuri kwenye Kikapu tofauti na zamani tulitambulika zaidi kwa soka'' - alisema Rajabu.

Temeke Heroes ambao wanafanyia mazoezi yao kwenye uwanja wa Bandari Club uliopo Kurasini, watashuka dimbani katika hatua ya robo fainali dhidi ya Portland Jumamosi ya Julai 21 ambapo pia mechi zingine 3 zikipigwa siku hiyo.

Mechi zingine za robo fainali ya michuano hiyo inayoandaliwa na East Africa Television LTD na kudhaminiwa na kinywaji baridi cha Sprite ni ile kati ya Mchenga Bball Stars dhidi ya St. Joseph, Water Institute dhidi ya Flying Dribblers na Team Kiza dhidi ya DMI. Bingwa atatwaa milioni 10,  mshindi wa pili milioni 3 huku MVP akihifadhi milioni 2.