Jumanne , 19th Feb , 2019

Shirikisho la soka nchini (TFF), kupitia kwa kamati yake ya Saa 72, imeitupilia kando rufaa ya Singida United dhidi ya Yanga iliyopinga vinara hao wa ligi kumtumia mchezaji Gustavo Simon.

Kikosi cha Yanga

Hilo limewekwa wazi na Afisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo alipofanya mahojiano na www.eatv.tv ambapo amesema rufaa hiyo tayari imeshatolewa maamuzi na kamati hiyo ya Saa 72.

''Kamati ilijiridhisha kuwa Gustavo Simon ni mchezaji halali wa Yanga na sio Dar City kama ambavyo Sungida United walilalamika, hivyo hakuna mabadiliko yoyote ya matokeo katika mchezo huo uliomalizika kwa suluhu'', amesema Ndimbo.

Mchezo huo ulipigwa Februari 6, 2019, kwenye uwanja wa Namfua mjini Singida na baada ya mchezo Singida walikata rufaa kuwa Gustavo ana leseni ya kuchezea klabu ya ligi daraja la pili Dar City FC na sio Yanga jambo ambalo kamati imelipangua na kusema ni mchezaji halali wa Yanga.