Alhamisi , 14th Mei , 2020

Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred amesema Shirikisho la soka Duniani FIFA, kila mwaka wanaipa Tanzania Bil 2.3 ambazo hutoka kwa awamu mbili yaani Januari na Julai na huwa unafanyika ukaguzi wa matumizi ya awamu iliyopita kabla ya kupewa tena.

Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred

Akiongea kupitia TFF TV leo Mei 14, 2020, Kidao amesema taarifa za matumizi mabaya ya fedha hizo zinazosambazwa si za kweli kwani fedha hizo hutolewa kwa kuzingatia vigezo na masharti.

''Moja ya masharti makubwa ya kupata fedha hizo ni kuwa na timu imara za taifa na ziwe zimecheza mechi za kimataifa zisizopungua 4, na hapa ni kwa timu zote ya wanaume, wanawake, U17, U20 na pia uwe na mfumo wa kisasa wa usajili #FifaConnect'', amesema.

Aidha Kidao amefafanua kuwa, ''Hizi fedha dola laki tano zinazosemwa zimeliwa ni zile ambazo ni awamu ya pili ya Bil 2.3 za kila mwaka, kilichobadilika mwaka huu Rais wa FIFA ameamua kuzitoa kabla ya Julai kwasababu ya janga la Corona ili kusaidiia mashirikisho''.

Pia amemshukuru Rais Magufuli kwa jinsi ambavyo amekuwa mstari wa mbele kuwasaidia kwenye kila jambo.

''Tunamshukuru sana Rais Magufuli kwa mchango wake wa Bil.1 kwenye maandalizi ya AFCON ya vijana, alitusaidia sana maana kwa kipindi hicho ilikuwa ngumu kutafuta vyanzo vya mapato kwingine na kufanikisha ila serikali ilitusaidia sana'' - Kidao Wilfred, Katibu Mkuu TFF.