Jumamosi , 16th Jun , 2018

Timu mbalimbali zilizojiandikisha leo kushiriki michuano ya mpira wa Kikapu ya Sprite Bball Kings msimu wa 2018, zimeeleza kufurahishwa na hatua ya kamati ya mashindano kuondoa kipengele cha 'Walk Over' kwenye mchujo.

Wakiongea kwenye usaili leo nahodha wa timu ya Portland ya Kinondoni Denis Babu na nahodha wa timu ya The Snipers Saleh Ramadhani, wamesema kanuni za mashindano msimu huu zimekuwa nzuri maana hakuna timu itavuka kwenye mchujo bila kupamabana.

''Mwaka jana sisi tulitolewa kwenye mtoano baada ya timu nyingi kupata 'Walk Over' pamoja na sisi kushinda lakini pointi zetu hazikutosha badala yake zikapita timu ambazo hazikucheza kutokana na wapinzani wao kutofika'', amesema Danis.

Naye Saleh amesema timu yake imejipanga kuhakikisha inapata pointi nyingi kwenye mchezo wa mchujo ili isije ikaishia hatua hiyo kama ilivyokuwa mwaka jana.

Kwa mujibu wa kamati ya mashindano mwaka huu timu zitalazimika kucheza mechi za mtoano ili kuingia kwenye 16 bora ambapo timu 15 ndipo zitaungana na bingwa mtetezi katika hatua hiyo. Lakini hakuna timu ambayo itapita bila kucheza hivyo kila timu iliyojisajili italazimika kucheza na kufuzu kwa wingi wa pointi.