Jumanne , 3rd Jul , 2018

Baada ya kufanyika kwa droo ya mechi za hatua ya 16 bora ya michuano ya Sprite Bball Kings hapo jana, timu ya Portland imeeleza majigambo yake na jinsi walivyotamani kukutana na bingwa mtetezi Mchenga Bball Stars.

Nahodha wa timu ya Portland Denis Babu.

Akiongea na East Africa Television, nahodha wa timu ya Portland Denis Babu amesema wapinzani wao timu ya Mbezi Beach KKKT watakiona cha moto siku ya Jumamosi kwenye uwanja wa Air Wing Ukonga kwani wao wamejipanga kumaliza mechi mapema tu.

''Yaani sisi tumeshajiandaa kwaajili ya kukutana na yeyote, imekuwa vizuri tumewajua wapinzani wetu ambao ni Mbezi Beach KKKT, niwaambie tu hawatuwezi wajiandae kuondoka'', amesema Babu.

Aidha Babu ameongeza kuwa wao kama Portland walikuwa wanatamani kupangwa na bingwa mtetezi Mchenga Bball Stars ili wawatoe kwenye hatua za mwanzo kama ilivyotolewa Ujerumani kwenye Kombe la Dunia.

Kwenye mchezo wa Mchujo Portland iliifunga Eagle Wing pointi 46 kwa 18 huku Mbezi Beach KKKT ikiifunga Oratory kwa pointi 32 kwa 20. Mechi za 16 bora zitapigwa Julai 7 na 8 kwenye viwanja vya Air Wings Ukonga na Bandari Kurasini.